Sunday, 25 May 2014

MBUNGE VICKY KAMATA AUGUA GHAFLA KABLA YA HARUSI YAKE YA KIFAHARI .

Mbunge Vicky Kamata akiwa amelazwa
Hospitali ya Tabata General, Dar es Salaam
jana.
Picha na Florence Majani



--- Ni matukio nadra kutokea katika maisha,
lakini haya ndiyo yaliyomkuta Mbunge wa Viti
Maalumu (CCM), Vicky Kamata, baada ya
kuugua ghafla saa 36 kabla ya harusi yake.
Kuugua kwa bibi harusi huyo mtarajiwa,
kumezua gumzo katika Viwanja vya Bunge mjini
Dodoma na maeneo mengine nchini, kutokana
na kile kilichoelezwa kwamba harusi hiyo
ilipangwa kuwa ya kifahari ikitarajiwa kutumia
Sh96 milioni.
Kamata ilikuwa afunge ndoa leo katika Kanisa
Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa
Mkombozi, Sinza Dar es Salaam na tayari kadi
za mialiko zilishasambazwa kwa watu
mbalimbali wakiwamo wabunge.
Habari za kuugua ghafla kwa mbunge huyo
ambaye pia ni msanii wa muziki aliyetamba na
kibao chake cha ‘Wanawake na Maendeleo’
zilianza kuzagaa kwa kasi juzi jioni nchini.
Kamata ambaye pia ni mtetezi wa haki za
wanawake, aliugua usiku wa kuamkia jana na
kupelekwa katika Hospitali ya Tabata General,
iliyopo Segerea ambapo amelazwa.
“Niliugua tumbo ghafla, nilipata maumivu
makali sana nikampigia daktari wangu na
nilipomweleza jinsi ninavyojisikia, aliniambia
niende hospitali haraka na kutokana na hali
ilivyo, waliamua nilazwe,” alisema Kamata
akiwa kitandani katika hospitali hiyo.
Kamata alifafanua kuwa, pamoja na mambo
mengine, hali yake ya ujauzito imekuwa
ikimsumbua na kuchangia yeye kulazwa kwa
mara ya pili sasa katika kipindi cha wiki mbili.
Mbunge huyo ambaye alitakiwa kufunga ndoa
leo, alisema kuwa kutokana na maradhi hayo,
haelewi hatima ya ndoa yake, ingawa
wanafamilia na wanakamati wanaendelea na
mipango ya harusi kama ilivyopangwa.

“Mama anaenda nyumbani sasa hivi kuniandalia
nguo na kila kitu, lakini sijui itakuwaje kwa
sababu daktari amesema kutokana na hali
yangu ilivyo, itakuwa vigumu kuvaa viatu virefu
na kupata usumbufu wote wa purukushani za
harusi,” alisema.
Aliongeza kuwa mipango yote ya harusi ipo
tayari kinachosubiriwa na siku yenyewe, lakini
kwa bahati mbaya jambo hilo limetokea na
haliwezi kuepukika.

Vicky alisema wanakamati wa Dar es Salaam na
wale wa Dodoma, wanaendelea na vikao ingawa,
wamechanganyikiwa kutokana na sintofahamu
iliyopo, kama harusi itafanyika au haitafanyika.
Ndugu wa mbunge huyo akiwemo mama yake
mzazi Kamata walionekana hospitalini hapo
wakiendelea kumfariji na kujadili kuhusu hatima
ya harusi hiyo, iliyokuwa ikingojewa kwa hamu
na wanafamilia wote.

Daktari wa Kamata, aliyefahamika kwa jina la
Diwani Msemo, alieleza kuwa mbunge huyo
alifika hospitalini hapo akiwa na maumivu
makali ya tumbo yaliyofanana na uchungu wa
kuzaa, hali iliyoonyesha kuwa ujauzito wake
unatishia kutoka.Ukipata yale maumivu kama
mimba ni changa inakuwa kama tishio la mimba
kutoka, siyo hivyo tu, bali alikuwa anatapika na
presha ikashuka. Kwa kweli mimba yake ipo
katika hatari,” alisema
Alisema pamoja na kumpa matibabu,
walishauriana kuwa apumzike kwa siku tano ili
kuhakikisha kiumbe kilichopo tumboni kipo
salama.

“Ilikuwa ni uamuzi mgumu kwa sababu ni siku
yake ya harusi, lakini tunaangalia umuhimu wa
kiumbe na kama ataenda, itabidi asaini ili
ijulikane kuwa hatukumkubalia. Kwa kifupi
hayuko fiti kwa shughuli hiyo,” alisema.
Harusi ya Kamata iliandikwa pia na mitandao
mbalimbali ya kijamii nchini na jana redio moja
ilitangaza kuugua kwake, ikisema kumetokana
na matatizo ya ujauzito.




Kumekuwa na uvumi unaosambazwa kwa kasi
juu ya sababu za kuahirishwa kwa harusi hiyo,
lakini kwa sababu ya maadili ya uandishi
hatutaweza kuziandika katika gazeti hili.
Paroko aliyekuwa afungishe ndoa anena
Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira
Maria Mama wa Mkombozi , Sinza Dar es
Salaam, Cuthbert Maganga alipohojiwa kuhusu
taarifa za kufungwa kwa ndoa hiyo, alikiri
kwamba iliandikishwa ili ifungwe kanisani hapo.

Hata hivyo akasema ilishindikana, baada ya
wahusika kukwama kuwasilisha baadhi ya
nyaraka muhimu zilizohitajika, ili kukamilisha
sakramenti hiyo.

“Ilitarajiwa kufungwa Mei 24 mwaka huu yaani
kesho (leo), lakini kwa taratibu za kanisa letu
ilishindikana kwa sababu bibi harusi alishindwa
kuwasilisha cheti chake cha ubatizo, pia
hakuwa amepata kipaimara, vitu hivyo ni
miongoni mwa vitu muhimu vinavyohitajika ili
kukamilisha Sakramenti ya Ndoa,” alisema
Padri Maganga.
Alisema Kamata ndiye aliyekwenda kuandikisha
ndoa hiyo, kwa kuwa ni muumini wa kanisa hilo
anayetokea Kanda D.
Juhudi za kumtafuta bwana harusi, Charles
Gardner hazikuweza kufanikiwa baada ya simu
yake kuita bila kupokelewa, hata alipotumiwa
ujumbe wa maandishi hakuwa tayari kujibu.

Hata hivyo, baadhi ya rafiki wa karibu wa
Gardner walieleza kuwa wamejulishwa kuwa
ndoa hiyo haipo na kwamba jana bwana harusi
huyo mtarajiwa alionekana akiwa katika hali
isiyo ya kawaida.“Nilijaribu kumuuliza kuhusu
harusi yake, lakini hakuwa tayari kunieleza
bayana, ila hayupo katika hali yake ya
kawaida,” alisema mmoja wa rafiki zake.

No comments:

Post a Comment