Tuesday, 27 May 2014

MAMBO YENYE THAMANI KWENYE MAPENZI.

NI siku nyingine tunakutana tena kwenye safu
yetu nzuri ya Love & Life. Lengo ni lilelile,
kupeana mawili matatu kuhusu maisha yetu ya
kimapenzi.Kila siku tunapaswa kujifunza zaidi
kuhusu uhusiano na mapenzi maana maisha yetu
hatuwezi kuwakwepa wenzi wetu hivyo ni vyema
kujua mbinu mpya kila wakati za kuwafanya
wenzetu wafurahie uwepo wetu.
Nimekuwa nikisisitiza mara kwa mara,
usimwonyeshe mpenzi wako kuwa hana thamani.





Mpe nafasi akueleze hisia zake. Kumsikiliza na
kujua kilicho moyoni mwake kutakurahisishia
kuishi naye kwa furaha maana utakuwa
unafanya mambo ambayo yanampendeza.
Rafiki zangu, sasa tuendelee na mada yetu
ambayo ilianza wiki iliyopita. Nilifafanua mambo
mengi ambayo ni muhimu sana kwa wapenzi.
Unajua kuna vitu ambavyo wengine wanaweza
kuvidharau na kuviona vya kawaida lakini kumbe
vina thamani kubwa sana.
Mfano wanawake wengi huwa bize kuhakikisha
wanaume wao wanakuwa wenye furaha na
wanajiona wapo peke yao kwenye uhusiano. Ni
jambo zuri, lakini kwa wanaume ni tofauti
kabisa.
Hawana muda wa kuangalia mambo ambayo
yanaweza kuwa kivutio kwa wenzi wao. Hilo ni
tatizo kubwa sana kwenye uhusiano. Kwa bahati
nzuri ni kwamba, wanawake huwa
wanafurahishwa na mambo madogo sana.
Wanapagawishwa na vitu vya kawaida sana
ambavyo vipo ndani ya uwezo wa mwanaume.
Hebu twende tukaone vitu vingine ambavyo
huwachanganya wanawake.

UJUMBE WA MAHABA
Kumtumia mpenzi wako au mkeo ujumbe wa
mahaba ni sehemu ya kumwongezea ‘uchizi’
katika penzi lenu. Wengi hawapendi na pengine
hawawezi kutunga meseji za kimahaba.
Kwa bahati nzuri ni kwamba, siku hizi za
utandawazi mambo ni rahisi sana, magazeti
mengi yanaandika Love Messages – za
Kiingereza na Kiswahili.
Achana na magazeti hata baadhi ya kampuni za
simu hufanya hivyo. Kwa gharama ndogo
unaweza kujiunga na huduma hiyo kisha ukawa
unatumiwa meseji kila siku.
Mitandao mbalimbali ya kwenye kompyuta nayo
huandika meseji mbalimbali. Kitu cha kufanya
hapo ni kukopi kisha kurekebisha kidogo kama
utaona kuna vitu vya kuboresha kidogo, kisha
mtumie mpenzi wako.
Unaweza kuona ni kitu kidogo sana, lakini utaona
atakavyozidi kukupaisha kithamani katika maisha
yake. Kama ulikuwa hujawahi kufanya, hebu anza
utaona faida yake.
Fanya hivyo kulingana na nyakati, mfano asubuhi
njema, mlo mwema, usiku mwema nk. Ni
utaratibu mzuri sana kimapenzi.



MITANDAO YA KIJAMII
Siku hizi kuna mitandao mingi ya kijamii. Kwa
bahati mbaya, baadhi ya watu huitumia vibaya
na kuanzisha uhusiano usiofaa huko. Wanawake
wengi huwa hawana amani na wanaume zao
hata kama kwenye maelezo yao ya utambulisho
wameandika wameoa au wana wachumba.
Kuweka picha yake mara chache au maneno ya
kuonyesha unavyompenda, huziba hisia zake
mbaya na kujiona yuko na mwanaume huru na
makini.
Lakini hata hivyo, utakuwa umejiwekea ulinzi
madhubuti na kuwafanya wanaofikiria kuwa na
wewe wabadili mawazo yao wakijua kuwa nafasi
imejaa! Jaribu utaona ukweli wa ninachokisema.

KUWA HURU NAYE
Wanaume wengi hawapendi mahaba, lakini
asikudanganye mtu, kuongozana na mwenzi
wako huongeza msisimko na kumfanya azidi
kuwa huru na mwenye kujiamini. Usimwogope,
mshike mkono, tembeeni huku mnamzungumza.
Kichwani hujiona mwanamke kamili, aliye na
mwanaume asiye na ‘vimeo’ mitaani. Haya ni
machache kati ya mengi ambayo kwa hakika
hustawisha penzi.

No comments:

Post a Comment