Pages

Pages

Pages

Wednesday, 28 May 2014

MAFUNZO.......ADHABU YA MZINIFU.(BASED ON ISLAMIC SHARIA).



UTANGULIZI.
Sheria imempitishia na kumuwekea
mzinifu aliye muhswani kwa kuoa/
kuolewa itakapothibitika kuwa katenda
jarima ya zinaa. Ikathibiti kwa njia za
kuithibitisha zilizowekwa na sheria
ambazo ni ama kukiri yeye mwenyewe
kutenda mbele ya kadhi au ushahidi wa
watu wanne waliomuona akitenda. Huyu
adhabu yake aliyowekewa na sheria ni
kupopolewa kwa mawe hadi kufa ingawa
wapo mafiqihi waliosema kuwa adhabu
yake ni viboko mia pamoja na
kupopolewa mawe.
3:2-ADHABU YA KURUJUMIWA (KUPIGWA
MAWE HADI KUFA):
Kabla hatujaingia kuizungumzia na
kuifafanua adhabu hii ya kurujumiwa,
hatuna budi kwanza kuleta ujulisho
(definition) wa huyu mzinifu muhswani
(mwenye ngome) ambaye ndiye
anayetekelezewa adhabu hii ya “Rajmu”,
ni nani. Halafu tena tutaje sharti za
“Ihswani”-ungome, kisha tubainishe
uwekwaji wa sheria hii na namna ya
kuitekeleza kwake.
a) Ujulisho wa Ihswani:
“Ihswani” ni neno la Kiarabu lenye
maana ya: Kuingia ndani ya ngome na
tunaposema “mtu muhswani”,
tunamaanisha: Mtu aliyeingia ndani ya
ngome yenye kumuhifadhi na kumlinda
na jarima ya zinaa . Na hakika si
vinginevyo mtu huwa muhswani
aliyeingia katika ngome imlindayo dhidi
ya zinaa kwa kuoa (mwanamume) na
kuolewa (mwanamke). Allah Taala
amesema: “...NA WANAPOINGIA
NGOMENI (kwa kuolewa)...” [4:25]
Husemwa katika lugha: Mwanamke
muhswani kwa maana ya mwanamke aliye
katika ndoa (aliyeolewa ndoa halali), kwa
kusawirisha kwamba mumewe ndiye
aliyemtia katika ngome (ndoa). “NA
WALIO KATIKA NGOME MIONGONI
MWA WANAWAKE...” katika aya inayo
bainisha wanawake walio haramu
kuwaoa, katika kauli yake Allah:
“MMEHARIMISHIWA (kuoa) MAMA
ZENU, NA WATOTO WENU, NA DADA
ZENU, NA SHANGAZI ZENU, NA NDUGU
ZA MAMA ZENU...” [4:23] Mapendeleo
na muradi wake ni wale wanawake
walioolewa.
b) Sharti zinazomfanya mtu kuzingatiwa
kuwa muhswani kisheria:
Mafaqihi wametaja sharti kadhaa mbali
na ndoa ambazo ihswani haitimii ila
kwa kukamilika/kupatikana kwake. Ziko
baadhi ya sharti ambazo
wamekongamana kwazo wote kwa
pamoja na nyingine wamekhitalifiana.
Tutazitaja sharti zote za ihswani, kisha
tutakuwa tunabainisha baada ya kila
sharti rai/maoni ya mafaqihi juu ya
kuifanya kuwa ni sharti au kinyume
chake. Tunaanza kuzitaja sharti hizo
kama ifuatavyo:-
I. AKILI: Ili wanandoa wote
wawili; mke na mume wazingatiwe kuwa
ni mtu muhswani ni lazima wawe na
akili timamu. Hili ni sharti kongamanwa
mbele ya maimamu wote wanne; Maalik,
Shaafiy, Ahmad na Abu Haniyfah-Allah
awawiye radhi. Itakapoharibika akili ya
mmojawapo wa wanandoa ,
hatazingatiwa na sheria kuwa ni
muhswani. Lakini huku kuharibikiwa
kwake kiakili hakutaathiri ihswani ya
mwenziwe mwenye akili timamu kwa
cho chote. Na ataendelea kuzingatiwa
kuwa ni muhswani chini ya kauli za
maimamu Maalik na Shaafiy [Rejea
SHAR-HUL-KHARSHIY ‘ALAA
MUKHTASWAR KHALIYL 5/323 na AT-
TAAJU WAL-IKLIYLU-6/275,276]. Lakini
mbele za maimamu Abu Haniyfah na
Ahmad Ibn Hambal, ihswani ya yule
mwingine itabatilika hata kama ana akili
timamu. [Rejea TAB-YIYNUL-
HAQAAIQ-3/173 na AL-
MUGHNIY-10/128]
II. BALEGHE: Hii pia ni sharti
kwa kila mmoja wa wanandoa ili
azingatiwe kuwa ni muhswani. Hali
kadhalika ni sharti kongamanwa mbele
za maimamu wote wanne: Maalik,
Shaafiy, Ahmad na Abu Haniyfah-Allah
awawiye radhi. Atakapokuwa hajafikia
baleghe mmoja wa wanandoa, sheria
haitamzingatia kuwa ni muhswani. Wala
huku kutokuifikia kwake baleghe
hakutaiathiri ihswani ya mwenza wake
aliye baleghe na ataendelea kuwa
muhswani kwa mujibu wa kauli ya
Imamu Shaafiy. [Rejea MUGHNIL-
MUHTAAJ-4/136]. Lakini hilo
litaibatilisha ihswani ya mwenziwe hata
kama yeye ni baleghe, hivyo ndivyo
waonavyo maimamu Maalik [Rejea
HAASHIYATUL-ADAWIY-5/323, Ahmad
[Rejea AL-MUGHNIY-10/128] na Abu
Haniyfah [TAB-YIYNUL-HAQAAIQ]
III. UISLAMU: Hili pia ni sharti
ambalo kupatikana kwake kutamfanya
kila mmoja wa wanandoa kuonekana
kuwa ni muhswani mbele ya macho ya
sheria. Na haya ndio madhehebu ya
maimamu Maalik [SHARHUL-KHARSHIY
5/323 na AT-TAAJU WAL-IKLIYLU
6/275,276] na Abu Haniyfah
[TABYIYNUL-HAQAAIQ 3/172].
Ikikosekana sharti ya ihswani kwa
mkewe (akawa si muislamu),
hazingatiwi kuwa ni muhswani na hivyo
kutoa nafasi ya kuifanya ihswani ya
mumewe kubatilika kwa sababu yake.
Lakini madhehebu ya Imamu Shaafiy
[AL-MUGHNIY 10/129] na Imamu Ahmad
katika kauli tegemewa [ZAADUL-
MA’AADI 3/207,208]. Uislamu sio sharti
ya ihswani kwa wanandoa ili
wazingatiwe na sheria kuwa ni
muhswani.
DALILI/HOJA ZA KILA KAMBI:
Imamu Maalik na Abu Haniyfah
wamesema kuwa ili kila mwanandoa
ahesabike kuwa ni muhswani kisheria ni
lazima awe muislamu kwa ushahidi wa
kauli hii ya Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie: “Ye yote
atakayemshirikisha Allah, basi huyo si
muhswani”. Ibn Is-haaq-Allah amrehemu.
Na maana ya kauli hii ni kwamba yeye
si mkamilifu wa hali, kwani muhswani
ni yule mkamilifu wa hali. Na adhabu ya
kurujumiwa kwa mawe haisimamishwi
(haitekelezwi) ila kwa yule aliye
mkamilifu wa hali atakapopatikana na
hatia ya dhambi ya zinaa. Na pia
imepatikana dalili kwamba Ka’ab Ibn
Maalik-Allah amuwiye radhi-alitaka
kumuoa mwanamke muyahudi. Mtume-
Rehema na Amani zimshukie-
akamwambia: “Muache (usimuoe), kwani
hakika yeye hakufanyi wewe kuwa ni
muhswani”. Ibn Abiy Sheibah,
Twabaraaniy, Daaruqutwniy & Ibn Adiy-
Allah awarehemu.
Ama dalili ya maimamu Shaafiy na
Ahmad juu ya kauli yao kwamba
Uislamu sio sharti katika kuzingatiwa
kila mmoja wa wanandoa kuwa ni
muhswani. Ni hadithi iliyopokelewa
kutoka kwa Ibn Umar-Allah awawiye
radhi-kwamba yeye amesema: “Mayahudi
walikuja kwa Mtume wa Allah-Rehema na
Amani zimshukie-wakamtajia ya kwamba
mwanamume na mwanamke miongoni
mwao (mayahudi wenziwao) wamezini.
Mtume wa Allah-Rehema na Amani
zimshukie-akawaambia: “Mnapata hukumu
gani katika Taurati (yenu) kuhusiana na
suala la Rajmu (kupopolewa kwa mawe)?”
Wakasema: Tunawafedhehesha na kisha
wanacharazwa bakora. Abdullah Ibn
Salaam akasema: Mmeongopa, hakika ndani
yake (Taurati) mna hukumu ya Rajmu.
Ikaletwa Taurati, ikafunguliwa, mmoja wao
akaiziba kwa mkono wake aya ya Rajmu.
Akaisoma aya iliyo kabla yake na ile ya
baada yake. Abdullah Ibn Salaam
akamwambia: Ondoa mkono wako,
akauondosha, tahamaki hiyo ndio aya
(inayotaja) Rajmu. Wakasema: Amesema
kweli Muhammad, imo ndani yake aya
inayotaja Rajmu. Mtume wa Allah-Rehema
na Amani zimshukie-akaamrisha
warujumiwe, wakarujumiwa. Basi
nikamuona mwanamume (mzinifu) yule
akimuinamia mwanamke (mzinifu mwenza)
kumkinga na mawe. Bukhaariy & Muslim-
Allah awarehemu.
Hadithi hii iko wazi katika kuonyesha
kuwa mazingatio katika kuwa mtu ni
muhswani au sio muhswani ni ndoa tu,
na adhabu ya Rajmu hutekelezwa kwa
msingi huu. Kama ambavyo hadithi
imefumbuliza kuwa Uislamu sio sharti
ya ihswani na kwa kuwa jinai ya zinaa
imelingana sawa baina ya muislamu na
asiye muislamu. Basi ni wajibu pia
walingane sawa katika adhabu. Pamoja
na hoja hii wako wanachuoni
wanaoipinga kwa kusema kuwa hadithi
hii haifahamishi kuwa Uislamu sio sharti
linalomfanya mwanandoa kuzingatiwa
kuwa ni muhswani. Kwa sababu Bwana
Mtume-Rehema na Amani zimshukie-
aliwahukumu Rajmu Mayahudi wale kwa
kufuata hukumu zilizomo ndani ya
Taurati na sio kwa mujibu wa Qur-ani.
Madai haya yamejibiwa ya kwamba
Mtume wa Allah aliwahukumu kwa
kufuata Qur-ani, haya ni kwa mujibu wa
kauli tukufu ya Allah: “NA
TUMEKUTEREMSHIA KITABU KWA (ajili
ya kubainisha) HAKI,
KINACHOSADIKISHA VITABU VILIVYO
KUWA KABLA YAKE, WALA USIFUATE
MATAMANIO YAO KWA KUACHA HAKI
ILIYOKUFIKIA. NA KILA (uma) KATIKA
NYINYI (binadamu) TUMEUJAALIA
SHERIA YAKE NA NJIA YAKE”. [5:48]
IV. KUPATIKANA TENDO LA NDOA
NDANI YA NDOA SAHIHI:
Hili ndilo sharti la msingi katika
kumzingatia kila mmoja wa wanandoa
kuwa ni muhswani mbele ya sheria.
Haya ndio madhehebu ya maimamu
wote wanne: Maalik [SHARHUL-
KHARSHIY 5/323], Shaafiy [MUGHNIL-
MUHTAAJ 4/125], Abu Haniyfah
[TABYIYNUL-HAQAAIQ 3/172] na Ahmad
Ibn Hambal [AL-MUGHNIY 10/126].

No comments:

Post a Comment