RAIS KIKWETE ASHINDA TUZO NYINGINE YA KIMATAIFA KATIKA UONGOZI.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa mara nyingine ametunukiwa tuzo la kimataifa.
Zamu hii kwa kuwa mshindi wa Tuzo la Nyota wa Demokrasia Afrika 2014 – Icon of Democracy Award Winner for 2014 in Africa.
Kwa mujibu wa barua aliyoandikiwa Rais Kikwete na kupokelewa Ikulu, Dar
Es Salaam, Rais Kikwete amekuwa mshindi wa kwanza, na kwa mbali kabisa
katika mchuano na marais watatu wa Afrika ambao walifikia mwishoni mwa
mchuano wa kuwania tuzo hilo.
Katika barua hiyo, Mchapishaji na Mhariri Mkuu wa Jarida hilo, Pastor
Elvis Iruh akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Tuzo 2014, amesema kuwa
uongozi wa Rais Kikwete umekuwa ni hadithi ya kusifiwa ya mafanikio
katika Bara ambako hadithi za namna hiyo siyo nyingi.
Tuzo hiyo hutolewa na Jarida la The Voice na mwaka jana mshindi alikuwa
ni Rais Bai Koroma wa Sierra Leone ambaye alikuwa ni mshindi wa pili wa
Tuzo hiyo ambayo ilitolewa kwa mara ya kwanza kwa Rais wa Kwanza wa
Zambia, Mzee Kenneth Kaunda.
Sherehe maalum ya kukabidhi tuzo hiyo imepangwa kufanyika Oktoba 17,
mwaka huu, 2014, katika Hoteli ya Van der Valk, iliyoko Almere,
Uholanzi.
Miongoni mwa sifa nyingine, Rais Kikwete anatunukiwa Tuzo hiyo kwa
sababu ya kuwa msimamizi mzuri na wa kweli wa demokrasia, kuendelea
kuhakikisha kuwa amani, utulivu na maendeleo vinaendelea kupatikana
katika eneo la Afrika ambalo limepitia vipindi vingi vya migogoro na
matatizo.
Aidha, gazeti hilo linasema kuwa Rais Kikwete amekuwa kiongozi wa mfano,
kimataifa na kikanda, na linatoa mfano wa mchango wake katika
kusuluhisha mgogoro mkubwa wa kisiasa nchini Kenya kufuatia uchaguzi
mkuu wa 2007.
Rais Kikwete pia anasifiwa kwa mchango wake katika kusimamia maendeleo
ya Tanzania katika nyanja mbali mbali – kilimo, elimu, miundombinu,
maendeleo ya viwanda, utalii na pia mchango wake katika kuendeleza
vijana na kutoa nafasi nyingi kwa akinamama kushika nafasi nyingi za
uongozi.
Jarida la The Voice pia limempongeza Rais Kikwete kwa kuimarisha Umoja
na Muungano wa Tanzania na kutoa nafasi kwa wananchi kujadili na
kukubaliana kuhusu Katiba mpya ya Tanzania.
Aprili mwaka huu, Rais Kikwete alitunukiwa tuzo la kuwa kiongozi mwenye
mchango mkubwa zaidi katika maendeleo ya Afrika kwa mwaka 2013 – The
Most Impactful Leader in Africa 2013.
No comments:
Post a Comment